Tanzania imesema kuwa itaimarisha biashara na nchi ya Uganda kwa lengo la kuinua uchumi wa raia wa mataifa hayo mawili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa tayari Tanzania imeanza kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo itakwenda pamoja na ujenzi wa bandari kavu Mkoani Mwanza ili kuwapunguzia muda wa usafiri wafanyabiashara wa Uganda wanaolazimika kusafiri hadi bandari ya Dar es Salaam kuchukua mizigo yao inayotoka nje ya nchi kwa meli.

Pia amesema kuwa serikali yake itakarabati meli ya MV Umoja itakayovusha mizigo hadi bandari ya Port Bell kupitia ziwa Viktoria, mbali na kununua ndege 6 za kusafirisha kwa ajili ya Shirika la ndege la Taifa (ATCL) na kupunguza vizuizi vya barabarani hadi kufikia 3.

Vile vile Rais Magufuli amesema Tanzania ipo tayari kuanzisha ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga baada ya kukamilisha mazungumzo ya masuala machache yaliyokuwa yaliosalia na ametaka wawekezaji waanze kazi badala kutoa visingizio.

Kwa upande wake Rais Museveni amemshukuru Rais Magufuli kwa mapokezi mazuri aliyoyapata akisema Uganda itaendelea kuwa ndugu na rafiki wa kweli wa Tanzania huku akisisitiza kuwa rafiki na ndugu wa kweli ni lazima wawe wamoja katika maamuzi na mipango mbalimbali ikiwemo maendeleo na biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *