Serikali za Tanzania na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara zilizokuwa zimewekeana kuhusu bidhaa kutoingizwa katika nchi hizo.

 Hayo yamezungumzwa na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Maiga katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Waziri Maiga amesema kuwa kuondolewa kwa vikwazo hivyo ni kuzingatia taratibu za kibiashara ambazo zilikubaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 Nchi hizo ziliwekeana vikwazo vya biashara ambapo Kenya waliweka vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG) kutoingia nchini humo na Tanzania iliweka vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara zinazozalishwa nchini Kenya.

 Waziri Maiga amesema kuwa kwa kuzingatia mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi hizi mbili na kwa kujali manufaa mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wakuu wa nchi hizi mbili Dkt. John  Magufuli na Uhuru Kenyatta wa Kenya walikubaliana kuviondoa vikwazo hivyo mara moja.

 Hatua hiyo ya kuondoa vikwazo hivyo ilifuatia maelekezo waliyotoa viongozi hao kwa mawaziri wao wa mambo ya nje, Dkt. Augustine Mahiga na Dkt. Amina Mohammed wa Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *