Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameziagiza hospitali zote za rufaa nchini ngazi ya Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wa fistula.
Waziri huyo aliyasema hayo mjini Tanga kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya wagonjwa wa fistula itakayodumu kwa kipindi cha wiki moja kuanzia juzi hadi Agosti 19, mwaka huu.
Pia waziri Ummy amesema tatizo la fistula limekuwa likiongezeka kila siku na waathirika wengi ni akinamama wa vijijini na wale wa kipato cha chini ambao wanashindwa kupata huduma sahihi za afya ikiwemo kuchelewa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa kujifungua.
Takribani akinamama 2,500 hadi 3,000 hupata tatizo la ugonjwa wa fistula kila mwaka japo idadi hii ni ndogo sana kuliko hali halisi ilivyo kwa kuwa wagonjwa wengi hunyanyapaliwa na familia zao na jamii kwa ujumla.