Shirika la Umeme Tanzania Tanesco limewatoa hofu wateja wake juu ya mfumo wa ununuzi wa Umeme kwa njia ya luku na kusema kuwa kwa sasa upo sawa na wanaweza kununua katika mifumo iliyozoeleka.
Kaimu Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano(TEHAMA) wa Tanesco, Demetruce Dashina alisema kuwa kulitokea tatizo dogo la mfumo wa ununuzi wa umeme kwa njia ya Luku kutokana na wataalamu wa shirika hilo walipokuwa wakihamisha mitambo hiyo kutoka ofisi ya Zamani kwenda sehemu nyingine.
Amesema kuwa shirika lilijipanga kuwahudumia wateja wake kama kawaida wakati wa kuhamisha mitambo hiyo lakini Wananchi wengi wakapata taharuki hivyo kufanya mfumo wa ziada kuzidiwa kutokana na watu kununua umeme kuliko Kawaida.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco Leila Muhaji aliwaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kuwasisitiza kuwa sasa wanaweza kununua katika mifumo iliyozoeleka.
Muhaji alisema kuwa Tanesco inatambua umuhimu wa umeme hivyo kuwataka watanzania kuwa na Imani na shirika lao kwani lipo kwa ajili ya kuwahudumia kama inavyohitajika.