Tamasha la Sauti za Busara linatarajiwa kufanyika kuanzia Februari 9 hadi 12 mwaka huu visiwani Zanzibar litawakutanisha wasanii zaidi ya 400 wa vikundi 40 vya muziki kutoka Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud amesema watu wajitokeze kwa wingi kupata vionjo vya muziki wa asili kutoka kwa wasanii mbalimbari barani Afrika kwani watapatiwa burudani za kiwango kikubwa.
Kauli-mbiu ya tamasha hilo mwaka huu ni “Africa United” ikiwa na maana kuwa muziki unaunganisha mtu na mtu, moyo na moyo ambapo katika dunia inayozidi kugawanyika, lugha ya muziki inahamasisha umoja na urafiki na mshikamano kwenye mipaka ya walimwengu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Sauti za Busara, Simai Said amewashukuru wadau wote kwa kuendelea kuliunga mkono tamasha hilo akisema uwepo wake unaendelea kusaidia fursa za kiuchumi na kuinua tamaduni za kiafrika duniani.
Naye Meneja wa tamasha hilo Ramadhan Journey amesema wasanii wote watatumbuiza moja kwa moja jukwaani hivyo kulifanya tamasha hilo kuwa la kipekee na tofauti kwani huonyesha uhalisia na ufanisi wa hali ya juu.
Kipaumbele cha tamasha hilo ni kuhakikisha kila shabiki anamudu kiingilio hivyo kwa Watanzania watalipa Sh. 6,000 kwa siku na kwa tamasha zima la siku nne watalipa Sh. 20,000.