Timu ya taifa ya Tanzania leo inashuka uwanjani dhidi ya Zambia katika hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya COSAFA Castle kwenye uwanja wa Moruleng nchini Afrika Kusini.
Zambia imefika Nusu Fainali baada ya kuitoa Botswana kwa kuifunga 2-1 Jumamosi, wakati Tanzania iliwatoa wenyeji Afrika Kusini kwa kuwachapa 1-0.
Mchezo wa nusu fainali kati ya Zambia na Taifa Stars umekuwa gumzo katika michuano hiyo kutokana na mafanikio ya Stars mpaka sasa kama timu waalikwa.
Mara ya mwisho Zambia na Tanzania kukutana katika michuano hiyo ni Julai 5 , 1997 jijini Arusha katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid na ‘ Chipolopolo ‘ ikienda sare ya 2-2 na Taifa Stars.
Timu hizo zimekwishakutana mara 30, Tanzania ikishinda mechi tano na Zambia ikishinda mechi 16, huku mechi tisa zikiisha kwa sare. Julai 5 kama leo, mwaka 1997 zilikutana katika Kombe la COSAFA pia na na zikamalizana kwa sare ya 2-2, lakini leo lazima mshindi apatikane.
Tanzania ilianzia hatua ya mchujo kwenye Kundi A ambako iliongoza kwa pointi zake tano sawa na Angola baada ya sare mbili 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius na ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi, hivyo kutengeneza wastani mzuri wa mabao na kuwapiku wapinzani kusonga Nusu Fainali.