Baada ya kuiangamiza Botswana, kesho Taifa Stars itashuka dimbani dhidi ya Burundi kwenye mechi ya kirafiki itakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa Jumamosi, Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa na Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya wa kikosi hicho, walishinda kwa mabao 2-0.

Burundi wametua nchini jana na kufikia Hoteli ya De Mag iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na jioni yake walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini.

Ndani ya kikosi hicho wamo washambuliaji wawili wanaotamba katika klabu za Simba na Young African za Dar es Salaam. Nyota hao ni Amisi Tambwe wa Young Africans na Laudit Mavugo wa Simba.

Kwa upande wake, Mayanga alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi iliyopita dhidi ya The Zebras ya Botswana na hivyo amehimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho.

Katika kuunga mkono wito wa Kocha Mayanga, TFF imebakiza viingilio vya mchezo huo kuwa sawa na vile vya Jumamosi iliyopita kwani katika mzunguko ambao unachukua mashabiki wengi kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *