Chama cha Wamiliki wa Mabasi Yaendayo Mikoani (Taboa), kimetangaza mgomo usio na kikomo kuanzia kesho, huku kikiwataka mawakala wanaotoa huduma za kukatisha tiketi kutofanya hivyo kuanzia leo.
Mgomo huo unalenga kupinga sheria zilizotungwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ambazo zinatajwa kuwa na vifungu kandamizi vinavyoweza kutishia ustawi wa biashara ya mabasi nchini.
Pamoja na hatua hiyo, wamiliki hao pia wamewataka wabunge kutopitisha sheria hizo hatari katika Bunge linaloanza keshokutwa.
Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alisema mgomo huo unalenga kuisisitiza Serikali na wabunge kwa ujumla kuhakikisha wanafuta baadhi ya vifungu vya sheria ambazo zitawaumiza wamiliki na wasafiri.
Alisema sheria zinazolalamikiwa ni pamoja na Sheria ya Leseni na Usafirishaji sura ya 317 namba 11 (6), ambayo ina kipengele cha adhabu ya kutaifisha magari kwa makosa ya binadamu .
Alisema adhabu ya kutaifisha magari haitawajenga wafanyabiashara hao, bali itawarudisha nyuma kimaendeleo, kwakuwa wengi wao wanaiendesha kwa mikopo.
Alisema mapendekezo yaliyotolewa katika kifungu namba 35(1) yana lengo la kuongeza adhabu ya faini kutoka Sh 10,000 hadi kufikia Sh 2,00,000, huku kosa la mara ya pili likitozwa kutoka kiwango cha juu cha Sh 20,000 hadi Sh 5,00,000.