Gavana wa mji wa Mombasa nchini Kenya, Hassan Joho ni miongoni mwa viongozi wa Nasa waliositishiwa hati za kusafiria nchini humo.
Hassan Joho ambaye ni swahiba mkubwa wa Alikiba na wenzake 14 wa viongozi wa Nasa wamesitishiwa hati zao za kusafiria baada ya kusapoti kuapishwa kwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, Raila Odinga mwezi uliopita.
Mbali ya Joho, wanasiasa wengine waliositishiwa hati zao za kusafiria ni seneta wa Siaya, James Orengo na seneta wa zamani wa Machakos, Johnson Muthama.
Mratibu mkuu wa mikakati wa Nasa, David Ndii pamoja na mfanyabiashara Jimi Wanjigi pia pia wamesitishiwa hati hizo za kusafiria.
Katika barua waliyopelekewa viongozi hao wanaodaiwa kufikia 15, Mkurugenzi wa Uhamiaji, Gordon Kihalang’wa alisema kusitishwa kwa hati hizo kumefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Wananchi na Uhamiaji ya mwaka 2011 inayotoa sababu za kusimamishwa.
Kwa upande wa Muthama alisema viongozi kutoka idara ya uhamiaji walitoa barua hiyo ya kumjulisha kuhusu hatua ya kusitishiwa hati ya kusafiria kuanzia saa 7:00.
Seneta huyo wa zamani ambaye pia ni kiongozi wa ngazi ya juu wa upinzani alisikitishwa kwamba njia zisizofaa zinazotumika kwake tayari zimemvuruga.
Nae kiongozi wa Nasa, Kalonzo Musyoka ameelezea kusimamishwa kwa hati za kusafiria kwa viongozi wa juu wa Nasa na kufungwa kwa vyombo vya habari kuwa ni sifa za serikali yenye hofu.