Serikali imesema ina mpango wa kufunga mfumo mpya maalum kwa ajili ya kuratibu na kudhibiti mwendo wa magari nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na ongezeko la ajali za barabarani.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu nchini (SUMATRA), Bw. Johansen Kahatano.
Amesema mfumo huo utatamika katika kuratibu mwendo wa magari hasa yale makubwa kwakuwa utaonesha ripoti kamili ya namna gari linavyokwenda mpaka kituo husika cha ukaguzi na unatoa urahisi kwa mamlaka husika kuchukua hatua kwa kuwa utarekodi muda wote wa safari.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Kebwe Steven Kebwe amesema katika kuhakikisha mkoa wake unapunguza ajali za barabarani wameanza kutoa elimu kuhusu usalama barabarani kuanzia shule za msingi hadi kwenye taasisi mbalimbali zilizopo katika mkoa huo.
Ameongeza kuwa mkoa wa Morogoro umekua ukikumbwa na matukio ya ajali za mara kwa mara kwa kuwa mkoa huo upo katikati ya nchi hivyo umepitiwa na barabara za kuelekea mikoa mbalimbali.