Spika wa Bunge la Uingereza, John Bercow amekosolewa kwa kupinga hatua ya rais Donald Trump kuhutubia bunge la taifa hilo wakati wa ziara yake.
Mwanachama wa chama cha kihafidhina amesema kwamba matamshi yake yamesababisha chuki huku mbunge mmoja akisema kuwa hayafai huku wengine wakidai hafai kupendelea upande mmoja.
Bercow alisema pingamizi dhidi ya ubaguzi wa rangi na ule wa kijinsia zinapaswa kuangaziwa sana na wanachama wa bunge hilo.
Mbunge wa Marekani Joe Wilson amesema kuwa ni pigo kwa chama cha Trump cha Republican.
Mwandishi wa maswala ya kisiasa Eleanor Garnier amesema kuwa ni pigo la kidiplomasia kwamba rais Trump hataruhusiwa kuhutubia bunge la nchi hiyo.
Mwezi uliopita waziri mkuu wa Uingereza Theresa May alisema kuwa rais Trump amekubali mwaliko kutoka kwa malkia wa Uingereza kwa ziara rasmi nchini Uingereza baadaye mwaka huu.
Lakini akizungumza bungeni siku ya Jumatatu bw Bercow alisema kuwa anapinga rais Trump kuhutubia mabunge yote kama ilivyo ada na viongozi wengine wa kimataifa.