Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amefunguka na kusema atakwenda jijini Nairobi nchini Kenya kumuona Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye anafanyiwa matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya kufuatia kupigwa risasi Septemba 7, 2017.
Ndugai kusema kuwa watakwenda kumuona Tundu Lissu kwani ni mbunge wao na wao wanampenda sana na kudai kuwa kipindi cha nyuma alishindwa kwenda Kenya kwa kuwa nchi hiyo ilikuwa kwenye uchaguzi na haikuwa na utulivu wa kisiasa ila kwa kuwa saizi imetulia anatarajia kwenda baada ya Christmas kumjulia hali.
“Mimi kama Spika siwezi kwenda na kutoka navyotaka Kenya bali napokwenda kule lazima kuwe na taarifa rasmi za kiserikali na kibunge na ninapokelewa hivyo na ninapopelekwa huko hospitali au wapi napelekwa kwa utaratibu huo ndiyo utaratibu wa nchi kwa nchi. Haiwezekani wao wana mechi kama zile (Uchaguzi) halafu spika nazunguka zunguka Nairobi wanaweza kusema ajenda aliyokuja nayo huyu siyo hii, katika pande hizi mbili Watanzania wamemtuma huyu ana ajenda nyingine kwa hiyo unapokuwa kiongozi lazima ujiongeze”.
Ndugai aliendelea kueleza kuwa “Haukuwa wakati mzuri kwenda Nairobi, ila kwa kuwa haya mambo yamepita na serikali saizi imekaa sawa sawa basi tusubiri Christmas ipite baada ya hapo mtamuona Spika muda si mrefu akienda kumuona Mbunge wake Nairobi au mahali pengine popote pale, yule ni Mbunge wetu na tunampenda sana na tusingependa asikitike kwa lolote lile”.
Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma na baadaye kupelekwa nchini Kenya jijini Nairobi kwa matibabu ambapo mpaka sasa yupo huko anaendelea na matibabu.