Kocha mpya wa Ivory Coast, Marc Wilmots amefanikiwa kumshawishi mchezaji wa timu hiyo Salomon Kalou arudi kuchezea timu ya taifa.
Mchezaji huyo ametajwa katika kikosi cha wachezaji 27 watakaochezea timu hiyo ya taifa.
Kalou, ambaye amekuwa akichezea Hertha Berlin, alistaafu baada ya timu hiyo kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu.
Kalou mwenye miaka 31 alikuwa ametangaza michuano hiyo ya Gabon ingekuwa yake ya mwisho lakini kwamba alikuwa anafikiria uwezekano wake kuchezea Ivory Coast hadi Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018.
Wilmot pia amefanikiwa kuwashawishi wachezaji wanne waliochezea timu ya vijana ya taifa la Ufaransa kubadili msimamo na kuamua kuchezea Ivory Coast.
Jean-Philippe Gbamin, Jeremie Boga na Maxwell Cornet wanaweza wakachezeshwa mara ya kwanza Juni. Seko Fofana anauguza jeraha.
Ivory Coast watakutana na Uholanzi mechi ya kirafiki Juni 4 na dhidi ya Guinea siku tano baadaye mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika.Mechi hizo zitakuwa za kwanza za Wilmots tangu kuteuliwa kwake Machi.