Klabu ya Simba imepigwa faini ya 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi yao dhidi ya Mbao FC iliyofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Adhabu hiyo imetolewa leo na kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba imevunja Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia Kamishna wa mechi hiyo, Maliki Tibabimale amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo hicho cha Simba.
Kwa upande mwingine kamati imeiadhibu Singida United sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Wakati huo Stand United imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,500,000 (milioni moja na laki tano) kutokana na makosa mawili kwenye michezo miwili tofauti ambayo ni Wachezaji kuvaa jezi zenye namba tofauti na zilizosajiliwa kwenye mechi dhidi ya Simba pamoja na mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Simba.
Kamati imeionya klabu ya Stand United endapo vitendo hivyo vitatokea tena haitasita kuichukulia hatua kali zaidi za kikanuni.