Beki wa Simba, Shomari Kapombe huenda akatemwa kwenye dirisha dogo la usajili kutokana na kushinwawa kuitumikia klabu hiyo tangu ligi ianze akisumbuliwa na majeraha.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba Zacharia Hanspope amesema klabu hiyo haiwezi kuendelea kumlipa mshahara mchezaji huyo bila kutimiza majukumu yake ya kucheza.
Hanspope amesema kuwa “Kapombe anatakiwa achague kucheza au kama hataki kucheza ahame mana vipimo vinaonesha amepona lakini yeye anaweza kuwa anaogopa kuumia, na huu mchezo unahitaji mtu atumie mwili sasa kama hajapona hauwezi kuendelea kumlipa mshahara”.
Kapombe aliumia July 15 mwaka huu kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu fainali za CHAN dhidi ya Rwanda uliopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Mlinzi huyo wa pembeni mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali za eneo la ulinzi alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea Azam FC lakini hajaichezea Simba msimu huu kutokana na kuuguza majeraha.