Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amepiga marufuku shule za binafsi na serikali kupokea wanafunzi bila kupimwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).
Pia Waziri Ummy ameagiza watu walio katika makundi hatarishi wakiwemo wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI na wajawazito wafike vituo vya Afya kupimwa Kifua Kikuu (TB).
Akitoa maagizo hayo leo Jijini Arusha kwenye maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani, Ummy alisema lengo la kupima makundi hayo muhimu ni kuzika kuenea kwa ugonjwa huo mapema, kwani mgonjwa mmoja ana uwezo wa kuambukiza watu 20 kwa mwaka kama hajaanza kutumia dawa kitu ambacho ni hatari.
Amesema tatizo ni kubwa nchini kwani takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Tanzania kwa mwaka 2015 jumla ya watu 160,000 waliugua Kifua Kikuu kati ya hao watu 62,180 sawa na asilimia 39 tu ndiyo waligunduliwa na kupata matibabu.