Tamasha hilo lilifanyika kwa siku tatu na na kila siku ilikuwa na muziki wake, ambapo lilianza siku ya kwanza na muziki wa taratibu, ikafuatiwa na siku ya muziki wa Hip Hop uliopewa jina la ‘African Massage’ na kisha kumaliziwa na siku ya muziki wa singeli uliohitimisha tamasha hili.
Kati ya wasanii waliopanda jukwani usiku huo ni pamoja na Dulla Makabila, Meja Kunta, Balobalo na Sholo Mwamba ambaye alionekana kuwafunika zaidi wenzake huku madansa wake 20 aliopanda nao jukwaani wakizidi kuunogesha usiku huo.
Sholo Mwamba pia katika usiku huo ndio msanii pekee aliyepanda mara mbili jukwaani na watu waliofurika viwanja vya Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TaSUba), ambako tamasha lilikuwa linafanyika wakionekana kutomchoka kwa kucheza naye mwanzo mwisho.
Mara ya kwanza msanii huyu alipanda saa tatu usiku ikiwa ni muda mfupi baada ya kuwasili mgeni rasmi ambaye ni Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye naye alionekana kufurahia shoo hiyo.
Kama haitoshi alipanda tena saa sita usiku na kuimba takribani saa nzima huku waliokuwa wakicheza nao akiwaambia watimue vumbi, jambo ambalo lilisababisha waliokuwa wamekaa kwenye viti kuondoka eneo hilo.
Akizungumzia shoo hiyo, Sholo Mwamba amesema muziki wa singeli raha yake ni amshaamsha, hivyo vyote alivyovifanya ni katika kuwapa mashabiki zake burudani.