Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Zanzibar limesema kuwa linahitaji jumla ya Sh bilioni 5 ili kukarabati na kuzifanyia matengenezo nyumba 26 zilizopo katika hali mbaya kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi humo.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Mohd Hafidh amesema hayo wakati alipokutana na uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na wataalamu wengine kutathmini hali ya majengo mbalimbali yaliyopo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Amesema baadhi ya majengo ya nyumba hizo ni zile zinazomilikiwa na Shirika la Nyumba la Serikali zilizokuwa nyumba za maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali imeweka malengo na mikakati ya kuufanya mji wa Zanzibar ikiwemo sehemu ya Mji Mkongwe kuwa kivutio cha watalii.
Amesema juhudi hizo ni pamoja na kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo yaliyopo Mji Mkongwe ambayo baadhi yake yapo katika hali mbaya ya uchakavu kiasi ya kutishia maisha ya wananchi.