Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amekanusha tuhuma kuwa alitoa maneno ya uchochezi alipozungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita.

Badala yake, Ponda amesema alitoa tahadhari kwa matukio yanayojitokeza na jinsi ya kuyakabili kwa mustakabali wa amani ya nchi.

Sheikh Ponda alishikiliwa na polisi kwa takriban siku mbili baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu safari yake ya Nairobi, Kenya alikokwenda kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika mkutano huo alizungumzia utekaji, kuokotwa kwa miili ya watu na mazungumzo aliyofanya na Lissu

Polisi walimhoji na kupekua nyumbani kwake wakituhumu kuwa alitoa maneno ya uchochezi.

Sheikh Ponda alisema: “Nilizungumza kwa nia nzuri kwa masilahi ya Taifa na umma. Nilikuwa nakumbushia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwamba vina wajibu wa kusimamia amani na usalama.

Kuhusu upekuzi uliofanyika nyumbani kwake Ubungo – Kibangu, Sheikh Ponda alisema hawakukuta chochote.

Sheikh Ponda, mwanaharakati wa haki za Waislamu, alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi Oktoba 13 asubuhi kwa wito wa kamanda wa Jeshi la Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam ambaye alimpa saa 72 kufanya hivyo.

Baada ya kujisalimisha alishikiliwa kwa mahojiano na baadaye askari walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake na aliachiwa Oktoba 14 akitakiwa kuripoti jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *