Serikali imezindua Mpango Kazi wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto unaolenga kushirikisha wadau katika jitihada za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa jamii inajukumu la kuhakikisha ukatili wa wanawake na watoto unapigwa vita kwa vitendo.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Kumekuwepo na matukio mengi ya ukatili yanayosababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini katika familia, mila na desturi potofu zenye athari katika jamii, malezi na makuzi mabovu na sheria kandamizi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Sihaba Nkinga amesema kuwa, kabla ya kuandaliwa kwa Mpango Kazi huu, Tanzania ilikuwa na mipango kazi minane (8) ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.