Serikali imetangaza kusimamisha kupokea wakimbizi kutoka nchi za Maziwa Makuu kwa makundi, kutokana na kutokuwepo kwa sababu za kiusalama, zinazowafanya wakimbizi hao kukimbia nchi zao na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba mjini Kigoma wakati wa uteketezaji wa silaha haramu, lililofanyika kikanda mkoani Kigoma, na kueleza kuwa kwa sasa hakuna tena wakimbizi watakaoingia kwa makundi watakaoruhusiwa kuingia nchini.
Mwigulu amesema serikali itawapokea wakimbizi mmoja mmoja na kila atakayeingia atahojiwa na mamlaka zinazohusika na mamlaka zikijiridhisha kuwa anastahili hadhi ya ukimbizi, atapokewa na kupelekwa kwenye kambi za wakimbizi zilizopo, kwani hakuna tena kambi ya wakimbizi itakayofunguliwa kwa sasa.
Amesema serikali kwa kutumia vyombo vyake, imejiridhisha kwamba hakuna hali mbaya ya usalama, inayowakimbiza raia hao kutoka kwenye nchi zao na kwamba zaidi imegundulika kuwa wengi wao wanakimbia kwa sababu za kiuchumi, kuja kutafuta namna ya kuishi ili kukidhi hali zao za maisha.
Amesema uwepo na uingiaji wa wakimbizi nchini, umekuwa na mchango mkubwa katika uzagaaji wa silaha haramu sanjari na kuongezeka kwa matukio ya utumiaji wa silaha na kuathiri uchumi na maisha ya watu mbalimbali.