Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo imesema itahakikisha utaratibu wa kusambaza pembejeo za ruzuku za mbegu na mbolea unatekelezwa vizuri, ili kuwafikia wakulima kwa wakati.

Aidha, serikali imesema pamoja na kwamba inatoa ruzuku ya asilimia 25 na wakulima wakilipia asilimia 75 iliyobaki, itaendelea kuangalia namna ya kumpunguzia mkulima gharama za pembejeo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo ya wabunge kama ilivyo utaratibu wake kila Alhamisi bungeni.

Majaliwa alisema serikali ina mpango mzuri wa kusambaza pembejeo kwa wakulima na itaendelea kuusimamia.

Waziri Mkuu amesema nia ya serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati kwa ruzuku ya asilimia 25 inayotolewa na serikali na itaendelea kuangalia namna ya kuweka unafuu zaidi kwa wakulima ili walipe fedha kidogo zaidi.

Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (CCM) aliyemuuliza Waziri Mkuu ana kauli gani kwa wakulima wa Mbeya ambao kuelekea msimu wa kilimo na mvua zimeanza kunyesha, lakini pembejeo hazijawafikia wakulima na zikifika zinachelewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *