Serikali imetangaza kurejesha michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi (UMITASHUMTA).

Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni mjini Dodoma, ambapo amesema mashindano hayo yanarudi na yatafanyika kitaifa mkoani Mwanza kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Ikumbukwe kuwa serikali kupitia Waziri wa TAMISEMI, Mh. George Simbachawene, mwaka jana alitangaza kusitisha mashindano hayo kwa muda usiojulikana, katika kipindi ambacho wahusika (wanafunzi, wachezaji na walimu) walikuwa tayari wamekwisha wasili Mwanza kwa ajili ya mashindano hayo.

Simbachawene alisema sababu ya kusitisha mashindano hayo ilikuwa ni kukithiri kwa ugonjwa wa kipindupindu pamoja na zoezi la madawati akidai kuwa waliokuwa wanahusika katika mashindano hayo ndiyo waliokuwa wakihusika katika zoezi lile la madawati, hivyo aliwataka walimu na watendaji wa halmashauri kuweka nguvu kwenye ukamilishaji wa zoezi la madawati kwanza kabla ya michezo hiyo.

Aidha waziri mkuu pia amewapongeza timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys kwa kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana, Twiga Stars kwa kuibuka mabingwa wa CECAFA na mwanariadha Alponce Simbu kwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Mumbai Marathon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *