Serikali imeombwa kudahili zaidi wanafunzi wa fani ya utoaji dawa ili waweze kusaidiana na wafamasia katika utoaji wa dawa sahihi kwa wagonjwa.
Akizungumza katika kongamano la wafamasia, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Michael Kishiwa amesema hivi sasa idadi ya Watanzania ni kubwa, lakini wataalamu wa dawa wakiwemo wafamasia ni 1,200, hatua inayochangia kuwepo kwa watoa huduma wasio na sifa.
Amesema kutokana na kukosekana wanataaluma, kumekuwepo na changamoto kubwa ya baadhi yao wanaotoa dawa kukiuka maadili na wengine kufanya kazi ya utoaji dawa pasipokuwa na uelewa nayo, hali ambayo ni hatari kwa afya za binadamu.
Kishiwa alisema kazi kubwa ya chama chao ni kuhakikisha kinasimamia ubora wa utoaji huduma ya dawa na kusimamia maadili, ili wananchi wapate dawa sahihi na kuzitumia ipasavyo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, amesema Serikali katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ya dawa, imeanza kufanya marekebisho ya sera ya uanzishwaji viwanda vya dawa nchini.