Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema, Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango mkubwa kuinua uchumi wa Taifa pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika lindi la umasikini.

 
Dk. Waziri Mpango ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani, wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi hiyo.
 
Amesema kuwa kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya Watanzania hivyo mapinduzi yanayokusudiwa katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya wakulima.
 
Kuhusu sekta ya Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa wataalamu wa Uchumi na Fedha katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia kupitia upya kodi zinazoleta kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.
 
Eneo jingine alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia Tanzania Mkopo na ruzuku utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, ili shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *