Serikali imesema iko tayari kupokea ushauri wa namna bora yakuimarisha utendaji wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kuwa azma ya Serikali ni kuendeleza Taasisi hiyo kwani bado inahitajika na madhumuni ya kuanzishwa kwake yana tija kwa Taifa.
Akizungumza wakati akijibu Hoja za Wabunge na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Waziri wa Elimu Sayansi na Teknplojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa Bado Taasisi hiyo inahitajika hivyo Serikali inaangalia namna ya kuiboresha na si kuivunja kama ilivyopendekezwa.
Akifafanua Prof. Ndalichako amesema kuwa Taasisi hiyo inaweza kuimarishwa zaidi ili kuendana na mahitaji ya sasa ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuimarisha na kukuza kiwango cha elimu nchini.
Akizungumzia mikakati yakuimarisha elimu nchini Profesa Ndalichako amesema kuwa kwa sasa Serikali inafanya ukarabati wa Shule Kongwe hapa nchini, vyuo vya Ualimu, na Ujenzi wa maktaba yakisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 2500 kwa wakati mmoja hiyo ikiwa ni sehemu ya miradi yakuboresha elimu inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii yalipendekeza kuwa TEWW ivunjwe ambapo Serikali imesema kuwa Bado Taasisi hiyo inahitajika na ina tija hivyo kitakachofanyika ni kuiboresha zaidi ili kukuza elimu hapa nchini na Si kuivunja kama ilivyopendekezwa.
Taasisi hiyo imeanzishwa kwa sheria namba 139 ya mwaka 1989 na iko chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.