Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imefanikiwa kushinda mabao 3-2 dhidi ya Congo – Brazaville katika mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya fainali za U17 Afrika mwakani nchini Madagascar.

Matokeo hayo yanaiweka njia panda kidogo Serengeti katika kuwania tiketi ya Madagascar, kwani wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi huo mwembamba katika mchezo wa marudiano Oktoba 2.

Mshambuliaji Yohana Oscar Nkomola aliifungia Serengeti Boys mabao mawili kipindi cha kwanza dakika ya 43 na 45, yote kwa jitihada binafasi akifumua mashuti mazuri baada ya kuwatoka mabeki wa Congo.

Congo walipata bao lao la kwanza dakika ya 71 kwa mkwaju wa penalty wa Langa-Lesse Percy uliotolewa na refa Nelson Emile Fred baada ya Mboungou Prestige kuchezewa rafu na Israel Patrick.

Issa Abdi Makamba aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Nkomola, aliifungia Serengeti Boys bao la tatu dakika ya 83 kwa jitihada binafasi pia akimtoka beki wa pembeni wa Congo.

Bopoumela Chardon akaifungia Congo bao la pili dakika ya 88 akimalizia krosi ya Ntota Gedeon kutoka kushoto.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *