Sarafu kubwa iliyotengenezwa kwa dhahabu yenye picha ya Malkia Elizabeth wa Uingereza, ambayo inathamani ya $4m (£3.2m) imeibiwa kwenye makumbusho nchini Ujerumani.
Sarafu hiyo kutoka Canada imeandikwa kuwa ya thamani ya $1m, lakini kwa sababu imetengenezwa kwa kilo 100 za dhahabu, thamani yake ni ya juu sana kwa kutumia bei ya sasa ya dhahabu.
Iliibiwa usiku wa jana kutoka makavazi ya Bode mjini Berlin na watu wasiojulikana na kusababisha taharuki.
Haijabainika ni vipi wezi walifanikiwa kuingia bila kugunduliwa na mtambo wa kuzuia wezi, na kisha wakafanikiwa kutoroka na sarafu hiyo ambayo nusu kipenyo chake ni cha nusu mita.
Sarafu hiyo inadaiwa kuwa nzito sana kiasi kwamba mtu mmoja hawezi kuibeba kutokana na uzito wake.
Ngazi ilipatikana imetupwa kwenye reli iliyo karibu na mji huo wenye makumbusho nchini Ujerumani.