Makamu wa Rais wa Samia Suluhu Hassan ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia jana kwa watendaji na viongozi waandamizi wa wilaya ya Ilemela kuhamia kwenye wilaya hiyo na kuacha tabia ya kukaa kwenye wilaya nyingine kwa kisingizio cha kukosa nyumba za serikali.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo katika hotuba yake kwa wananchi na watendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi jengo la utawala la manispaa hiyo na kukabidhi madawati 1,074 yaliyotolewa na ofisi ya Bunge.

Akiwa katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wakati anaweka jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato jijini Mwanza, Makamu wa Rais aliuagiza uongozi wa jiji la Mwanza kusimamia kikamilifu mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato na kwamba watendaji watakaobainika kuhujumu mradi ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo katika hotuba yake kwa wananchi na watendaji wa jiji la Mwanza waliohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato unaohusisha uboreshaji wa jengo la machinjio, tangi la kuhifadhi maji, ujenzi wa vyumba vya baridi vya kuhifadhi nyama na ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka yanayotoka kwenye machinjio hiyo.

Makamu wa Rais pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhakikisha anasimamia uundaji wa menejimenti ya machinjio hiyo ambayo itaboresha utendaji kazi wa machinjio hiyo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *