Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi bonde la Ziwa Victoria.
Aliyasema hayo jana jijini Mwanza alipofungua kongamano la kisayansi la siku mbili lililohudhuriwa na wanasayansi na watafiti kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na wenyeji Tanzania.
Makamu wa Rais amesema kuwa Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu kwa wananchi wa nchi za Afrika Mashariki kwa sababu ni chanzo cha ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo na ni chanzo kubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya watu kwa nchi hizo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dk Ally Matano alisema Ziwa Victoria linakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile uchafuzi unaotokana na shughuli za viwanda, shughuli za kiuchumi kando ya ziwa na gugumaji.
Katibu amesema kuwa nchi wanachama zinazofanya kazi kupitia Bonde la Ziwa Victoria zimechukua hatua kadhaa katika kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwa na sheria na sera za pamoja kwa nchi wanachama ambapo baadhi ya changamoto hizo zimeanza kushughulikiwa.
Ameongeza kuwa, mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili tafiti mbalimbali zilizofanywa na watalaamu ili kubadilishana uzoefu na namna bora ya kutunza ziwa hilo sambamba na kujadili changamoto zinazolikumba ziwa hilo.