Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amemtumia ujumbe maalum Rais Dkt. John Magufuli akishukuru kwa jitihada za serikali ya Tanzania za kusaidia kupatikana kwa amani katika nchi hiyo.
Ujumbe huo wa Rais huyo umewasilishwa nchini na waziri wa biashara na viwanda wa nchi hiyo, Stephen Dhieu Dau Ayik kwa makamu wa rais Bi. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo amesema kwa sasa hali ya usalama inazidi kuimarika kufuatia kusitishwa kwa mapigano ya wanajeshi watiifu wa Salva Kiir na wanajeshi watiifu wa aliyekuwa Makamu wa rais Riek Machar.
Kwa niaba ya Rais Magufuli, Bi. Suluhu amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha amani inapatikana katika Taifa hilo changa barani Afrika ambapo itawezesha wananchi kufanya kazi kwa maendeleo kwa amani na utulivu.
Makamu wa rais pia amezitaka pande zote mbili zinazopingana kuzingatia na kuheshimu mkataba wa amani waliosaini jijini Arusha mwaka 2015 uliolenga kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kurejesha amani katika taifa hilo.