Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema uteuzi aliyoufanya Rais John Magufuli kwa kiongozi wa Chama cha ATC Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ni sahihi.

Sadiki aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, Rais hajakosea kumteua Mghwira kuwa kiongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwani mwana mama huyo ni mchapakazi, mzalendo na asiye na ubaguzi, na uongozi unahitaji mtu wa aina hiyo.

Amesema kuna maeneo matano ambayo angependa mteuliwa huyo ayape kipaumbele ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Amesema kama mazingira yataharibiwa zaidi ndani ya miaka 10 mkoa utakuwa jangwa na na kukumbwa na baa la njaa.

Katika eneo hilo, alitaka Mghwira ashirikiane na taasisi na viongozi wengine kutunza mazingira na vyanzo vya maji.

Pia amesema mkoa unakosa mapato mengi kutokana na mbinu za ujanja za wafanyabiashara wasio waaminifu. Alimtaka kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujipanga vyema kudhibiti hilo. Dawa za kulevya Alisema kuwa zimekuwa zikiathiri maendeleo ya mkoa.

Akatolea mfano Same ambako mirungi inalimwa sana na kumtaka alishughulikie huku akiwataka wananchi kumpa ushirikiano kuwafichua wanaofanya biashara hiyo haramu.

Kuhusu mimba mashuleni ameeleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana hadi Februari mwaka huu wamepatikana wanafunzi 38 wenye mimba kwenye wilaya ya Same pekee.

Amesema kwa kuwa mama Mghwira ni mwanamke, anayo nafasi ya kuzungumza kwa ndani na mabinti na wanawake wasikatishe masomo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *