Baada ya msichana kujitupa baharini alipokuwa ndani ya boti kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja ndugu wa msichana huyo wafunguka mazito kuhusu kisa hicho.

Kisa cha binti huyo mwenye umri wa miaka 16 kujitupa baharini akiwa katika boti ya Kilimanjaro V akitoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar juzi, kinaanzia kwenye mawasiliano yake na mvulana mmoja, kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, imefahamika.

Msichana huyo alikuwa akiwasiliana na mvulana huyo ambaye walifahamiana kupitia Facebook, kwa kutumia simu ya mkononi.

Akizungumza kwa huzuni, mama mdogo wa msichana huyo, Asha Saleh Mandhi, alisema palitokea mzozo baina yake na binti huyo baada ya kumkuta na simu ya mkononi wakati wazazi wake hawajamnunulia.

Amesema Jumatano iliyopita majira ya jioni akiwa nyumbani hapo na baada ya kupata taarifa kuwa mtoto wake wa kumlea anamiliki simu, alimwita na kumtaka aeleze amepewa na nani la sivyo atampeleka polisi akajieleze.

Amesema siku ya pili yake asubuhi, msichana huyo alitoroka nyumbani na ndipo alipotoa taarifa kituo cha polisi Madema kuwa amepotelewa na mtoto.

Mama mdogo huyo alisema baada ya kuwa ametoroka, aliichukua simu hiyo na kuangalia mawasiliano yake na ndipo alipofanikiwa kupata jina la kijana mmoja wa kiume ambaye alikuwa anawasiliana naye mara kwa mara. Hakumtaja.

Alisema baada ya kumpata kijana huyo kwa njia ya simu, aliulizwa anamfahamu vipi binti yao na kujibu kuwa wamejuana kupitia Fecbook, lakini hawajawahi kuonana kwa sababu yeye anaishi Dar es Salaam na binti anaishi Zanzibar.

Alisema alimpa taarifa kijana huyo kuwa binti yao ametoroka na haijulikani alikokwenda, hivyo kumwomba kusaidiana kuhakikisha wanampata akiwa salama.

Alisema aliwasiliana na dereva huyo ambaye alimueleza kuwa amesharipoti katika serikali ya mtaa katika eneo analoishi kuwa amemwokota binti huyo bandarini, Dar es Salaam baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kupata msaada.

Mama mdogo huyo alisema mama mzazi wa binti huyo anaishi Muscat, Oman na kwamba amemlea tangu akiwa mdogo.

Alisema walipata mshtuko baada ya kupata taarifa kuwa binti yao amejitupa baharini wakati akitokea Dar es Salaam baada ya kusakwa kwa siku kadhaa na hatimaye kupatikana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *