Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Mbunge wa jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ kutokana na vurugu zilizotokea eneo la Mgodi wa GGM Septemba 14 mwaka huu.
Mbunge Msukuma na madiwani wa wilaya ya Geita walifunga barabara zinazoingia kwenye mgodi wa GGM wakishinikiza kulipwa dola 12 milion zinazotokana na kodi ya huduma.
Kamanda wa polisi mkoani hapa Mponjoli Mwabulambo jana alithibitishwa kukamatwa kwa Msukuma na kusema askari walimkamata katika eneo la CCM mjini Geita. Kamanda amesema kukamatwa kwa Musukuma ni mwendelezo wa Polisi kuwakamata watu wote waliohusika katika vurugu zilizotokea Septemba 14.
Amesema tayari wamekamata madiwani wengine wawili na wananchi watano na kwamba jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi na msako wa kuwakamata wote walioshiriki.
Kamanda amesema kwa sasa wanaendelea na mahojiano na wakikamilisha sheria itachukua mkondo wake na kwamba kosa la jina halina kikomo na wote walioshiriki vurugu za kufunga barabara lazima wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria .
Hadi sasa jeshi la polisi mkoani Geita linawashikilia madiwani kumi wa halmashauri za wilaya ya Geita waliofunga barabara zinazoingia mgodi wa GGM na kuharibu miundo mbinu ya maji yaliyotengenezwa na GGM kwa ajili ya shughuli za mgodi na wananchi wa mji wa Geita katika kijiji cha Nungwe jambo ambalo ni kinyume na sheria.