Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema kuwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ndio inayoongoza kwa vitendo vya rushwa kisekta nchini.

Waziri huyo amebainisha kuwa Mahakama ya Ufisadi iko mbioni kuanza kazi, baada ya Jaji Mkuu kukamilisha kutengeneza kanuni za uendeshaji pamoja na mafunzo kwa majaji.

Kairuki amesema kwa mujibu wa mchanganuo wa kesi zilizopo mahakamani kisekta kuanzia Juni mwaka huu, zinaonesha mamlaka hiyo na sekta ya afya ndio zinaongoza kwa kuhusishwa na vitendo vya rushwa.

Amesema mchanganuo huo unaonesha kuwa hadi Juni mwaka huu, kesi zilizopo mahakamani za kisekta ni 509 na kati ya hizo kesi 209 sawa na asilimia 41 zinaihusu Serikali za Mitaa na kufuatiwa na sekta ya afya ambayo ina kesi 63 sawa na asilimia 12.

Pia amesema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuzuia na kupambana na rushwa katika eneo hilo hilo la mamlaka ya serikali za mitaa kutokana na kuongoza kwa kuwa na tuhuma na kesi nyingi za rushwa zinazoendelea mahakamani.

Kuhusu hatua za kuanzishwa kwa Mahakama ya Ufisadi zilipofikia, Kairuki alisema mahakama hiyo ipo mbioni kuanza kazi na mashauri yake yatachukua muda wa miezi tisa kusikilizwa na kutolewa maamuzi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *