Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amesema kuwa alikuwa anajua mipango ya ndoa ya Zamaradi Mketema.
Ruge amezungumzia suala hilo ikiwa ni wiki kadhaa tangu isambae sauti iliyoaminika kuwa ni ya kwake, akisikika mtu anazungumza na Zamaradi kwenye simu huku akilia kwa sauti ya mateso akilalama kuachwa.
Amesema kuwa kama mwanaume muungwana, huwa hazungumzii masuala ya ndani ya mahusiano yake ya kimapenzi.
Ruge amesema kuwa alikuwa anafahamu kila kilichokuwa kinaendelea kuhusu ndoa ya Zamaradi na kwamba alikuwa amempa baraka zote tofauti na ilivyokuwa ikizungumzwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ameshtukizwa na kuumizwa.
Ruge ameeleza kuwa hata wikendi iliyopita alikuwa na watoto wake aliozaa na Zamaradi na kwamba anawapenda sana na hataacha kumheshimu mama yao.
Amesema amelazimika kulizungumzia hilo ili kuweka kumbukumbu sawa na sio vinginevyo.
Zamaradi alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Take One cha Clouds TV. Alikifanya kipindi hicho kuwa maarufu huku akishiriki kuandaa filamu zilizoshika mitaa ikiwemo filamu ya ‘Kigodolo’.