Mahakama ya Rufani nchini, imefuta rufaa mbili za Jamhuri dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), baada ya Mawakili wa Jamhuri kudai hawana nia ya kuendelea na rufaa hizo.
Rufaa hizo namba tisa na 10 za mwaka huu, zilikuwa zinasikilizwa mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Benard Luanda, Jaji Musa Kipenka na Jaji Stella Mugasha ambapo Serikali iliwakilishwa na Wakili Paul Kadushi na Faraja Nchimbi huku Lema akiwakilishwa na Peter Kibatala na Adam Jabir.
Mawakili hao wa Jamhuri waliieleza mahakama hiyo kuwa wanaomba kuwasilisha ombi hilo ambapo baada ya jopo hilo la majaji kupitia kwa kina kwa sababu zisizozuilika wameona hawana nia ya kuendelea na rufaa hizo.
Mawakili wa Lema waliieleza Mahakama hiyo kuwa hawana pingamizi na maombi hayo kwani waliowasilisha rufaa hizo ni za Jamhuri wenyewe ila wanasikitishwa na vitendo hivyo vya mawakili wa serikali.
Jaji Luanda alikemea hatua hiyo na kuwaeleza mawakili hao kuwa wanaitia najisi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwani kila kitu kiko wazi na kufanya wanasheria wote waonekane hawana akili hivyo kuwataka kushikilia watu kwa misingi ya kisheria.
Hatua ya kufutwa kwa rufaa hizo katika kesi mbili za uchochezi zinamzomkabili mbunge huyo, sasa jalada la kesi hiyo linatarajiwa kurudishwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kuendelea na uamuzi wa kupata dhamana.
Source: Mtanzania