Mwanariadha wa Kenya, David Rudisha amefanikiwa kutetea ubingwa wake wa mbio za mita 800 kwenye mashindano ya Olimpiki yanayoendela nchini Brazili.
Rudisha ambaye alitwaa medali ya dhahabu jijini London, mwaka 2012 amefanikiwa kumaliza mbio hizo kwa dakika moja na sekunde 42.15.
Rudisha mwenye miaka 27 ameshinda mbio hizo kwa kumbwaga mpinzani wake Alfred Kipketer ambaye pia ni raia wa Kenya ambaye hata hivyo hakufanikiwa kushika nafasi tatu za juu licha ya kuongoza kwa umbali wa mita 500 za mwanzo.
Mkimbiaji wa Algeria, Taoufik Makhloufi alishika nafasi ya pili kwa kumaliza mbio hizo kwa dakika moja na sekunde 42.61 huku mmarekani Clayton Murphy akijiwekea rekodi binafsi na kumaliza nafasi ya tatu kwa 42.93.
Licha ya kushangaza watazamaji kwa kukimbia kwa umbali wa mita 200 kwa sekunde 23 tu, lakini Kipketer aliishia kumaliza kwenye nafasi ya saba.
Rudisha ameweka rekodi nyingine kwa Afrika kwa kuwa mkimbiaji wa kwanza kuweza kutetea medali ya dhahabu yam bio hizo tangu alipofanya hivyo mwanariadha wa New Zealand, Peter Snell mwaka 1964 kwa kutetea medali ya dhahabu kwa wanaume.