Mwanariadha, Mo Farah amekuwa mkimbiaji wa kwanza wa Uingereza wa mbio za uwanjani kushinda nishani tatu za dhahabu katika michezo ya olimpiki baada ya kuwashinda wakenya na waethiopia kwa kushinda mbio za mita 10,000 mjini Rio.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33 alijikwaa wakati wa mbio hizo, japo alijikaza katika mita 100 za mwisho na kushinda kwa muda wa dakika 27 sekunde 5.
Mkenya Paul Tanui ameshinda nishani ya fedha, huku mwanariadha wa Ethiopia Tamirat Tola akimaliza wa tatu.
Farah atarejea uwanjani jumatano ijayo kutetea taji lake la mbio za mita 5,000, aliloshinda miaka minne iliyopita mjini London nchini Uingereza.
Mwanariadha huyo kama atashinda mbio hizo atafikia mafanikio ya mwanariadha wa Finland Lasse Viren aliyehifadhi mataji mawili ya olimpiki katika mbio za mwendo mrefu mwaka wa 1976.