Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa baadhi ya watu wanaohusishwa na tuhuma za biashara ya dawa za kulevya wanaodaiwa kuwa marafiki zake, ni watu anaokutana nao ‘bila kupanga’ katika maeneo anayotembelea.
Ridhwani amesema hayo jijini Dar es Salaam baada ya kufanyiwa mahojiano na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, na kukanusha kuwa na uhusiano wa aina yoyote na watuhumiwa hao ingawa amekiri kuwa ‘huwa inatokea’ wao kujikuta wako kwenye eneo hilo hilo ambalo yeye ametembelea.
Amesema vita ya dawa ya kulevya ni kubwa na inapaswa kupigwa na kila mmoja ili kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanaathirika kutokana na suala hilo na kwamba kuhojiwa kwake kumemfanya awe na amani.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa jamii inapaswa kusimama kwa kauli moja ili kuliokoa Taifa na nguvu kazi inayopotea ili Taifa liwe na vijana wanaojitambua na kutimiza wajibu wao katika kulitumikia taifa.
Ridhiwani amesema mchakato huo wa kupambana na dawa za kulenya nchini umekuwa ukiwachanganya wananchi kwani haieleweki ni nani anayehusika na kushugulikia suala hilo.