Imekuwa ni kawaida ya vyombo vingi vya habari duniani hususani vyombo vinavyoripoti masuala ya burudani kujikita katika kutafuta namna ya kuwapa umaarufu wasanii au kujitengenezea umaarufu vyenyewe kupitia wasanii.
Ni kama mchezo wa ‘Nikune, nikukune’ kwakuwa mkono wako hauwzi kufika mgongoni kwako na mkono wangu hauwezi kufika mgongoni kwangu lakini mkono wa yeyote baina yetu unaweza kufika kwenye mgongo wa mwenzake.
Wasanii wanavitegemea vyombo vya habari kuwasaidia kupata umaarufu wakati huo huo vyombo vya habari vinawategemea wasanii ili kuimarisha biashara zao, nani anaumia? MLAJI, MTEJA, SHABIKI na MFUATILIAJI WA BURUDANI.
Katika hali ya kushangaza sana baadhi ya vyombo vya habari vya Tanzania vimekuwa mstari wa mbele kwenye kuandika kuhusu kukosekana kwa maelewano baina ya wasanii kuliko kuandika kuhusu mafanikio waliyonayo au namna walivyo na ushawishi kwenye mustakabali wa jamii ya Tanzania.
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tetesi za kuwepo ukosefu wa maelewano miongoni mwa wasanii wakubwa wa Tanzania hali inayopelekea hata hatua za msingi za ukuaji wa sanaa kwa wasanii hawa kubezwa na kudharauliwa ili tu tija ya mafanikio hayo isionekane kwa lengo la watu wachache waendelee kunufaika na taarifa za maendeleo ya migogoro hiyo.
Ni wazi kuwa kwa muda mrefu mastaa Ali Kiba na Diamond Platnumz wamekuwa wakivumishwa kuwa na uhasama ambao hata chanzo chake hakijulikani na athari ya uvumi huu ni kuwa mashabiki wa wasanii hawa wanawachukia na kuchukia au kudharau mafanikio ya msanii wasiyempenda bila kujua kuwa kufanya hivyo ni kudidimiza sanaa ya Tanzania.
Kwa hoja gani kubwa mtu anaweza kubeza mafanikio ya Ali Kiba yaliyopelekea kupata mkataba na kampuni kubwa ya Sony Music? Kwa hoja gani kubwa mtu anaweza kubeza hatua ya Diamond Platnumz kuanzisha record label yake na kusainisha wasanii kadhaa?
Lakini kwakuwa vyombo vya habari vimekuwa vikisisitiza kwenye kauli ambazo sio za msingi na zisizo na tija kwa sanaa ya Tanzania, kila kauli ya wasanii hawa kuhusu muziki na mafanikio yao imetafsiriwa kuwa dongo kwa mwenzake.
Ukweli wa mambo ni kuwa si Ali Kiba wala Diamond Platnumz aliyewahi kujitokeza na kudai kuwa ‘Yeye ana BIFF na mwenzake’ na kwakuwa huo ndio ukweli; Kwanini vyombo vya habari vimeendelea kuripoti kutoelewana baina ya wasanii hao?
Wafuatiliaji wa burudani watakapoacha kuwa wateja wa habari za uzushi wa migogoro miongoni mwa wasanii wao na wakaamua kuwa wafuatiliaji wa mambo mengine, vyombo hivi vitatoa habari gani?
Wasanii JITOKEZENI HADHARANI mkanushe hizi tetesi kwakuwa zinawaumiza mashabiki wenu kwa namna nyingi!