Walimu mkoani Shinyanga wamepigwa marufuku kufanya biashara ya kubeba abiria kwa piki piki maarufu kama ‘boda boda’ na badala yake wajikite zaidi katika kuinua elimu mkoani humo.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack wakati akizungumza na waratibu wa elimu kata, wakuu wa shule na manispaa na maofisa wa elimu wa mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa mkoa huyo amesema kuwa amesikitishwa na tabia ya baadhi ya walimu mkoani humo kugeukia biashara ya kuendesha bodaboda badala ya kufundisha, akisema hali hiyo inachangia kushuka kwa kiwango cha taaluma kwa wanafunzi.

Bi Talack amewaonya na kusema atakayebainika akiendelea kufanya shughuli hizo badala ya kufundisha, atafukuzwa kazi mara moja.

Kikao hicho kililenga kuwahamasisha walimu kuongeza juhudi za ufundishaji mwaka huu mkoani Shinyanga.

Amewaagiza wakuu wote wa shule kuacha kutoa ruhusa za hovyo kwa walimu badala yake wawabane ili wafundishe wanafunzi na kuongeza ufaulu.

Pia amewataka wakuu hao kuandaa daftari la walimu kusaini mahudhurio mara mbili, wakati wa kuingia shuleni na wakati wa kutokao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *