Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amezitaka halmashauri za mkoa huo kutumia vizuri fursa ya Serikali kuhamia hapo badala ya kuiachia manispaa pekee.

Rugimbana amewaeleza viongozi katika wilaya ya Mpwapwa kuwa, halmashauri zinatakiwa kuchangamkia fursa sanjari na manispaa.

Rugimbana amesema, amepokea maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu kwamba kila halmashauri ijipange na iweke matumizi bora ya ardhi na ipime viwanja vingi kwa lengo la kujiandaa kupokea watumishi wa serikali wanaohamia mkoani Dodoma.

Amesema, jukumu la kupanga mipango miji, lisiachiwe kuweka manispaa ya Dodoma peke yake, hivyo kila halmashauri ijiandae kwa kupanga miji yake vizuri.

Amezitaka zipange mji kwa kugawanya maeneo kwa shughuli mbalimbali ili kuondoa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza kutokana na kuingiliana katika matumizi yake.

Amesema kila halmashauri ijiandae kwa kuwa itatumika kama makazi ya watendaji watakaohamia mkoani humo, hivyo kwa kutojipanga maana yake ni kuipoteza fursa hiyo.

Rugimbana alipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuweka mkakati wa kupima viwanja, lakini akaonya kwamba wananchi waliochukuliwa mashamba yao, wanatakiwa kupewa kipaumbele katika mpango huo mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *