Rais na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Shimon Peres amefariki dunia leo akiwa na umri wa miaka 93 baada ya kusumbliwa na ugonjwa wa kiharusi.
Ripoti zimesema hali yake iliimarika kabla kuwa mbaya ghafla Juzi. Mtoto wake wa kiume, Chemi ameongoza maombolezo ya kiongozi huyo aliyeelezwa kuwa mmoja wa baba wa taifa la Israel aliyejitahidi bila kuochoka kupigania taifa hilo.
Viongozi kadhaa duniani akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani, Mwanamfalme wa Uingereza Charles na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Peres mjini Jerusalem Septemba 30.
Peres alikuwa mmoja wa kizazi cha mwisho cha wanasiasa wa Israel waliokuwepo wakati wa kuundwa upya kwa taifa hilo mwaka 1948.
Alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1994 kwa juhudi zake za kusimamia mikataba ya amani na Wapalestina mwaka mmoja kabla.
Aliwahi kusema Wapalestina ni majirani wa karibu zaidi wa Israel na huenda wakawa marafiki wa karibu zaidi wa taifa hilo la kiyahudi.
Peres amefariki dunia hospitali karibu na mji mkuu wa Israel, Tel Aviv mapema leo huku familia yake ikiwa kando yake.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema amehuzunishwa mno kutokana na kifo cha Peres.