Rais wa Uturuki, Recep Erdogan amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na niaba yaRais Magufuli.
Rais huyo ameambatana na mkewe Mama Emine Erdogan pamoja na Mawaziri watatu ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Uchumi Mheshimiwa Nihat Zeybekekci na Waziri wa Nishati na Maliasili Mheshimiwa Berat Albayrak
Pia Rais huyo ameambatana na wafanyabiashara wapatao 85 wa nchi hiyo ambao wamekuja kwa ajili ya kujionea masuala ya biashara nchini.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara na uwekezaji.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Erdogan atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.