Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi ameondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili aliyoifanya hapa nchini kwa mwaliko wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais huyo ameagwa na mwenyeji wake Rais Magufuli katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Internatinal Airport (JNIA) pamoja na viongozi wengine wa kiserikali hapa nchini akiwemo makamu wa Rais, Samia Suluhu na Waziri mkuu Kassim Majaliwa.
Rais huyo ameelekea nchini Rwanda ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akiwa hapa nchini Rais huyo amefanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha nyama nchini, ukuzaji wa sekta ya utalii pamoja na usafiri wa anga.
Kwa upande wa Rais Magufuli amemshukuru Rais huyo kwa kukubali kushirikiana nae katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa nchi hizo mbili.