Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ametangaza kujiuzulu urais wa nchi hiyo baada ya chama chake cha ANC kuanzisha vuguvugu la kumng’oa madarakani.
Zuma amesema asingependa damu imwagike na chama(ANC) kimeguke kwa sababu yake hivyo ameamua kuachia ngazi.
ANC kikiongozwa na Cyril Ramaphosa, siku chache zilizopit kilituma ujumbe maalum kumtaka rais huyo kuachia madaraka, kutokana na harakati nyingi za kumtaka afanye hivyo tangu mwaka jana.
Jacob Zuma anakabiliwa na tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ambapo Bunge la nchi hiyo kujaribu kupiga kura za maoni ili kumuondoa lakini ilishindikana, ndipo chama kikafanya mkutano na kuchukua uamuzi huo mgumu wa kumtaka afanye hivyo, la sivyo kitamtoa kwa nguvu.
Zuma amefuata nyayo alizopita rafiki yake mkubwa Robert Mugabe ambaye alikuwa Rais wa Zimbabwe, aliyetakiwa kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka 2017 na jeshi la nchi hiyo, la sivyo lingetumia nguvu kumng’oa, na hatimaye kuachia madaraka.