Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ameanzisha kampeni ya mchakato wa kufanyika kwa kura za maoni kujaribu kubadilisha katiba itakayompa nafasi ya kuongeza mihula mingine miwili baada ya kikomo cha utawala wake  mwaka 2020.

Rais Nkurunziza amesema hayo jana jumanne wakati akihutubia wafuasi wake katika kijiji cha Gitega huku akiwaonya wale wote watakaopinga juhudi zake kwa maneno au kwa vitendo watakuwa wameuvuka mstari mwekundu.

Kampeni hiyo maalumu yenye lengo la kumuweka Nkurunziza hadi mwaka 2017 imeanzishwa baada ya serikali kuzindua juhudi za kuchangisha fedha za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Viongozi wa upinzani wanaoishi uhamishoni wanasema kura hiyo ya maoni itakuwa kama mazishi kwa muafaka wa utiaji saini wa mkataba wa amani wa mwaka 2000.

Mkataba huo wa amani ulisaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13 na kusababisha vifo vya watu 300,000.

Burundi ilitumbukia kwenye mzozo mwingine wa kisiasa mwaka 2015 pale Rais Nkurunziza alipokataa kung’atuka madarakani baada ya kumaliza muhula wake na  kuwania tena urais.

Nkurunziza anakuwa Rais wa Pili Afrika Mashariki kuonesha nia ya kubadili katiba ili apewe muda mwingine wa kuongoza baada ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame kufanya hivyo mwaka 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *