Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Morogoro kuwaacha wafanya biashara ndogondogo wa mji huo waendelee kufanya biashara katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi wa Mororgoro eneo la Msamvu na kumueleza kero ya kunyanyaswa na Manispaa ya mji huo ambapo wamekuwa wakiwafukuza maeneo hayo.
Rais Magufuli amemuagiza kamanda wa Polisi wa mkoa huo, SACP, Urich Onesphory Mtei kuhakikisha askari mgambo hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo huku akiwataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.
Kwa upande mwingine Rais Magufuli amewataka watu waliobinafsisha viwanda mkoani humo kuvirejesha serikalini endapo wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajila.
Pia Rais Magufuli amewapongeza wakulima wa mazao mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao huku akiwataja wakulima wa Kilosa wakiongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 hadi kufikia asilima 82.