Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba  Julai Mosi mwaka huu.

Maonesho hayo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) yanayoanza rasmi Juni 28 hadi Julai 8, 2017 yakishirikisha makampuni toka nchi zipatazo 30.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema maonesho ya mwaka huu yamelenga zaidi kusaidia wajasiriamali wadogo ili kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda.

Ndiyo maana lengo la maonesho haya ni kuwapa fursa wafanyabiashara kuonesha bidhaa zao na si kuuza, ili wanapomaliza maonesho wapate wateja na fursa pana zaidi.

Amesema kila siku ya maonesho imetengwa kwa shughuli maalumu ya kumsaidia mshiriki kujiimarisha kibiashara, zipo siku za mazungumzo baina ya wafanyabiashara, siku za kukutana wafanyabiashara wa ukanda huu wa Afrika Mashariki na siku ya kujadili bidhaa.

Pia Waziri huyo amesema banda la bidhaa za ngozi litakuwa na shughuli maalumu ya kueleza faida ya bidhaa zitokanazo na ngozi pamoja na Gereza la Karanga kueleza azma ya kutengeneza soli za viatu na kuzisambaza nchini.

Awali akimkaribisha Waziri Mwijage, Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Edwin Rutageruka alisema washiriki watumie maonyesho hayo kutangaza bidhaa zao badala ya kufikiria kuuza lakini pia wabadilishane ujuzi na wafanyabiashara wa kimataifa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *